
Katika mkakati wake wa kuwainua wakulima nchini Kampuni ya Tanzania Breweries (TBL),
imewezesha wakulima wa zao la shayiri Kanda ya Kaskazini inaoshirikiana nao, kushiriki
maonesho ya kilimo yaliyofanyika Arusha yaliyoandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini
(TARI).
Meneja Kilimo wa TBL, Joel Msechu alisema kampuni imedhamini wakulima wapatao 100
kuhudhuria maonesho hayo kwa ajili ya kujifunza mbinu za kilimo cha kisasa na matumizi ya
teknolojia katika kuleta mapinduzi ya kilimo ili ziwasaidie kuongeza uzalishaji. Alieleza kuwa kwa
kipindi kirefu, kampuni hiyo imekuwa ikishirikiana na wakulima wa zao hilo kwa kuwapatia mbegu
bora, zinazofaa katika hali ya hewa ya maeneo yao na kuwahakikishia soko la uhakika wa mavuno
yao. Hatua hiyo imewezesha wakulima hao kuongeza uzalishaji.
“Kwetu TBL tunaamini ushirikiano unaweza kuchochea kuleta maendeleo endelevu. Maonesho ya
kilimo ni moja ya fursa ya kuwakutanisha wakulima wetu wa mazao ya shayiri na mtama na
kuwawezesha kupata maarifa ya kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo katika kazi
yao”,alisema Msechu.
Kampuni ya TBL imedhamiria kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania, za kuleta mapinduzi
ya viwanda kupitia kuwekeza katika sekta ya kilimo ambapo inashirikiana na wakulima 6,000 wa
zao la shayiri katika mikoa ya Kilimanjaro, Manyara, Arusha na Iringa. Pia, kampuni inajenga
kiwanda cha kusindika kimea mkoani Dodoma, ambacho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani
32,000 za kimea.
0 Comments